WAFANYA BIASHARA KARIAKOO WAGOMA.
Dar es Salaam.
Hadi saa 4.10 asubuhi hali ni tofauti na siku zote katika soko maarufu la Kariakoo ambapo maduka yamefungwa, hakuna msongamano wa watu katika mitaa yake wala kelele za wamachinga wakipishana kuuza bidhaa zao.
Huo ni utekelezaji wa msimamo wa wafanyabiashara wa Kariakaoo ambapo wameazimia kuanzia leo Jumatatu Mei 15, 2023 wanafunga maduka yao kwa ajili ya kushinikiza Serikali kuingilia kati kuanzishwa kwa sheria na tozo wanazodai zinazowakandamiza ikiwemo zile zinazotaka stoo walizonazo kusajiliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko hilo, Martin Mbwana amejitoa katika kile kinachoendelea Kariakoo kwa kusema yeye ni mjumbe wao tu hivyo watakachoamua ndiyo watafanya.
Jambo hilo liliwafanya wafanyabiashara eneo hilo kushangilia kwa sauti huku wakisema mwisho wa kuonewa umefika.
Awali majira ya saa 2 asubuhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alifikia katika soko hilo na kuzungumza na wafanyabiashara hao huku akiwataka wajumbe kusafiri nae kwenda Dodoma kwa ajili ya kikao na Waziri Mkuu jambo ambalo baadae katika kikao cha wafanyabiashara peke yao lilikataliwa.
Hiyo ni baada ya wafanyabishara kusimamia kile wanachokitaka kwa kudai kuwa hawawezi kufungua biashara zao hadi watakaposikilizwa kero zao na Rais au Waziri Mkuu aje sokoni hapo na sio wao kwenda Dodoma kwa kuwa wanalipa kodi.
Kwa upande wa huduma na biashara leo imekuwa siku ngumu kwa wachuuzi wadogo ambao hulitegemea soko la Kariakoo kuchukua bidhaa kwani wamekosa huduma baada ya maduka yote kufungwa tangu asubuhi.
No comments