Dodoma.
Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kampuni za simu nchini kuweka gharama nafuu ya vifurushi vya simu, ili wananchi wa vipato vyote wanufaike na huduma hizo.
Rais Samia ametoa kauli hiyo jana jijini hapa, ikiwa ni moja ya maagizo saba aliyotoa kwenye hafla ya utiaji saini wa mikataba ya kupeleka huduma ya mawasiliano vijijini, huku akiupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuwa umefanya mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya UCSAF iliingia mkataba na kampuni tano kwa ajili ya kujenga minara 758 ya mawasiliano vijijini ambayo kwa sehemu kubwa inakwenda kupunguza tatizo la kukosekana kwa mawasiliano, huku kata 58 zikikosa ukandarasi baada ya kuelezwa kuwa zina idadi ndogo ya wateja.
Mbali na hayo, mradi huo utanufaisha vijiji 4,708 vyenye watu milioni 8.5 katika kata 713 za wilaya 127 nchini.
Katika hotuba yake, Rais Samia amewataka watoa huduma kujali maisha ya watu, hasa wa vijijini ili wafikiwe na huduma za mawasiliano, ikiwemo kufunga teknolojia rahisi katika baadhi ya kata ambazo zilitajwa kuwa na wateja wachache, hivyo kampuni za simu kutoona umuhimu wa kuwekeza.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema utekelezaji wa mikataba hiyo ni miezi 18 kuanza sasa na wanatarajia itakuwa hivyo, lakini akabainisha kuwa Watanzania 15 milioni walishafikiwa na mawasiliano.
Waziri alisema tangu kuanza kwa mpango huo, Serikali imeshatoa ruzuku ya Sh199.9 bilioni ambayo huwa ni asilimia 40 na watoa huduma hutoa asilimia 60.
Hata hivyo, alisema kata 58 hazijapata makandarasi wa kujenga minara kutokana na watoa huduma kuona kuna idadi ndogo ya wateja, hivyo hawakuomba kujenga huko.
Kwa mujibu wa Nape, gharama za kujenga mnara mmoja ni kati ya Sh300 hadi Sh350 milioni, jambo linalosababisha wachague maeneo ambayo yanakuwa na wateja wa kutosha. Alisema wamedhamiria ifikapo 2025 kila kijiji Tanzania kiwe na mawasiliano.
No comments