Samia asema tufanye kazi ya kuirudisha nchi kwenye umoja.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuna kazi ya kuirudisha nchi kuwa moja baada ya kutetereka kwa watu kujuana kwa udini, kabila, ukanda na itikadi.
Rais Samia ameyasema hayo kwenye mdahalo wa kitaifa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, uliofanyika katika shule ya Uongozi Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema wakati wa enzi za Mwalimu alihakikisha anajenga taifa lenye umoja na mshikamano kwa kupinga ubaguzi wa aina zote ikiwemo rangi, dini, kabila, ukanda itikadi nk.
“Hapa pana kazi kubwa ya kufanya na panaumiza kichwa kidogo, nirudie tu maneno ya Abubakari Lyongo kwamba katikati hapo tulitetereka na tukanza kujuana kwa rangi, kwa dini , kabila, ukanda lakini pia na itikadi kwa hiyo tuna kazi ya kurudi kuifanya Tanzania kuwa moja pamoja na yote haya tuilokuwa nayo,” amesema Rais Samia.
Aidha amesema Mwalimu Nyerere amewaachia somo kubwa Watanzania la kuwa wazalendo na Taifa kwani alilipenda taifa lake, na kujitoa mhanga kwa ajili ya watanzania.
“Uzalendo wa Mwalimu Nyerere ulijidhihirisha tangu nyakati za kupigania uhuru, ambapo aliamua kuacha kazi yake ya ualimu ili ajikite zaidi kwenye kazi za kupigania uhuru na atukomboe Watanzania wenzie na akapitia magumu na changamoto nyingi kwa ajili ya kulikomboa taifa hili,” amesema Rais Samia.
Kuhusu lugha ya Kiswahili, alisema Mwalimu Nyerere aliiwezesha kukubalika wa Waafrika na sasa ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (Unesco) kuitengea siku yake maalumu.
No comments