Bocco kuikabili Mbao FC?
HABARI njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba, straika wao, John Bocco yupo fiti na yupo tayari kuikabili Mbao FC katika mchezo dhidi yao utakaochezwa keshokutwa Jumatatu.
Simba itaikaribisha Mbao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ulioteka hisia za mashabi wengi ukizingatia katika mchezo wa kwanza, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Daktari wa Simba, Yasin Gembe ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Bocco yupo fiti kucheza mechi dhidi ya Mbao baada ya kupona jeraha la enka aliloumia katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui FC.
Kutokana na jeraha hilo la enka, Bocco aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Azam FC, hakuweza kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti.
Gembe alisema: “Bocco yupo vizuri, amepona na anaweza kucheza mechi yoyote iliyo mbele yetu lakini jukumu la kumpanga kucheza linabaki mikononi mwa kocha.
“Kuhusu wachezaji wengine wote waliobakia wapo vizuri na wanafanya mazoezi kama kawaida majeruhi pekee aliyebakia kwetu ni Haruna Niyonzima ambaye yupo nchini India kwa matibabu.”
Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma akizungumzia kurejea kwa Bocco, alisema; “Bocco bado yupo nusu kwa nusu anaendelea kuimarika akiwa sawa uwanjani atacheza dhidi ya Mabao.”
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Mbao, Solly Nyashi alisema hawana hofu na Simba sababu wamejiandaa bila kujali ukubwa wa timu na lengo lao ni kushinda.
No comments