Picha : KIVULINI YAADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA NA WATOTO KWA KUFANYA MDAHALO WILAYANI KISHAPU
Shirika la Kivulini linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto leo Ijumaa Disemba 8,2017 limeadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto kwa kukutanisha wadau wa haki za wanawake na watoto katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kwa ajili ya kujadili namna ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mgeni rasmi katika mdahalo huo uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu alikuwa mkuu wa polisi wilaya ya Kishapu, SP Emmanuel Galiyamoshi.
Mdahalo huo uliolenga kujadili masuala mbalimbali ya ukatili wa kijinsia na watoto umehudhuriwa na maafisa maendeleo,afya,ustawi wa jamii,elimu,watendaji wa kata na vijiji,mratibu wa mama na watoto, polisi,viongozi wa dini,polisi na jeshi la jadi sungusungu.
Akifungua mdahalo huo, mkuu wa polisi wilaya ya Kishapu SP Emmanuel Galiyamoshi alisema ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wadau wote hawana budi kuungana pamoja na kila mmoja akitimiza wajibu wake.
“Ukatili dhidi ya wanawake na watoto upo,ili kuumaliza lazima kila mdau atomize wajibu wake,elimu itolewe,kesi zipelekwe mahakamani na wahusika watoe ushahidi,kupitia dawati letu la jinsia na watoto tumejipanga vyema kusaidia watu wote wanaofanyiwa vitendo vya kikatili”,alisema.
Galiyamoshi alilipongeza shirika la Kivulini kwa kutetea haki za wanawake na watoto huku akiliomba kutanua huduma zao na kusaidia pia wanaume ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili katika familia zao.
Naye Afisa mwandamizi wa mradi wa usawa wa kijinsia kujenga uwezo kiuchumi kwa wanawake na vijana kutoka shirika la Kivulini Bi. Eunice Mayengela alisema shirika hilo limeamua kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto wilayani Kishapu ili kuangalia hali halisi ya masuala ya ukatili wilayani humo.
“Maadhimisho haya ya siku 16 za kupinga ukatili kufanyika kila mwaka ambapo wanaharakati kote duniani huungana kwa pamoja kupinga ukatili na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Ukatili dhidi ya wanawake haumuachi mtu salama,chukua hatua’ ",aliongeza.
Mayengela alisema takwimu zinaonesha kuwa kati ya wanawake 10 waliofanyiwa ukatili,watatu pekee wanatafuta kwa kutoa taarifa polisi.
“Asilimia 54 ya wanawake wanaofanyiwa ukatili wanatafuta msaada kwenye familia na asilimia 9 pekee wanatafuta msaada polisi”,aliongeza Mayengela.
Wakichangia hoja katika mdahalo huo,wadau walisema ili wahanga wa ukatili wa kijinsia waweze kusaidiwa ndani ya saa 72,ni vyema jamii ikapewa elimu kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa kwenye vituo vya polisi na ofisi za kata matukio yanapotokea.
Aidha waliomba mazingira ya kutolea taarifa kuwa rafiki kwani vitendo hivyo ni vya aibu na watu wengi wamekuwa wakihofu kuwa wakienda baadhi yao huombwa fedha ili wapewe huduma.
Pia walishauri serikali za mitaa kuwa na ajenda ya kuduma kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia lakini pia kutunga sheria ndogo ndogo za masuala ya kijinsia.
Walizitaja sababu zinazosababisha ukatili dhidi ya wanawake na watoto kuwa ni pamoja na umaskini,ukosefu wa elimu,kukosa hofu ya mungu lakini pia wazazi kutotimiza wajibu kwa watoto wao.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MDAHALO HUO
Mgeni rasmi Mkuu wa Polisi wilaya ya Kishapu SP Emmanuel Galiyamoshi akifungua mdahalo wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto katika wilaya ya Kishapu leo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga
No comments