KANISA LA ASKOFU GWAJIMA LABOMOLEWA USIKU
Kufuatia zoezi la serikali la kupanua na kuboresha miundo mbinu mbalimbali nchini hususan ya barabara katika jiji la Dar es Salaam ambapo imelazimu baadhi ya maeneo kubomolewa ili kupisha zoezi hilo la upanuzi, Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima nalo limekumbwa na kadhia ya kubomolewa.
Kanisa hilo lililoko jirani kabisa na Barabara ya Morogoro ambayo serikali imepanga kuipanua ili kurahisisha usafiri na kupunguza foleni, lilitakiwa kubomolewa kutokana na kuwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara hiyo.
Mchungaji Biyagaza wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko chini ya Askofu Gwajima, ameeleza kuwa serikali iliwapatia notisi ya siku 30 ili wabomoe kipande cha jengo la kanisa hilo kilichopo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara.
“Ni kweli tunayo notice ya mwezi mmoja ya kuhakikisha kwamba eneo ambalo ni hifadhi ya barabara tunaliacha. Na hifadhi ya barabara ni mita 90 kuanzia katikati. Bahati nzuri wale waliokuja kuweka alama zao walipofika hapa na wahandisi , mafundi na baadhi ya watu wa kanisani walikuwepo. Basi tukawaambia wapime mita 90 zinapoishia. Kwa hiyo wakapima mita 90 zilipoishia wakaweka alama, wakasema basi nyie mnaweza mkabomoa upande huu na upande huu mkauacha kwa ajili ya hifadhi ya barabara,” alisema Mchungaji Biyagaza.
“Sisi baada ya hapo tukaona tujipange kwa ajili kuachia eneo la barabara ili shughuli nyingine ambazo ni mpango wa maendeleo ya serikali ziweze kuendelea na sisi tuweze kuendelea na eneo letu vizuri. Kwa hivyo kile kipande chote ambacho ni cha barabara na tukaongeza ndani kidogo chote tumekiondoa. Na hili eneo linalobaki tunapaimarisha ili nyumba ya Bwana iweze kufanya kazi yake ya kutoa huduma za kiroho,” aliongeza.
Mchungaji Biyagaza alieleza japokuwa eneo la jengo limepungua, eneo lililobakia linaimarishwa ili kanisa hilo liweze kuendelea kutoa huduma za kiroho kwa waumini wake.
Aidha kufuatia zoezi hilo la upanuzi wa barabara ya Morogoro ambalo linaenda sambamba na ujenzi wa barabara za juu (fly-over) katika makutano ya barabara eneo la Ubungo, umepelekea kubomolewa kwa majengo mbalimbali ikiwemo majengo ya wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na jengo la Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania ambayo yamebomolewa kufuatia agizo la Rais Dkt. John pombe Magufuli.
No comments