TUMBATU FM

Breaking News

Jicho la 3: Mzamiru ‘stuka’ unategemewa Simba, Stars

KWA yeyote aliye mfuatiliaji wa mpira wa miguu nchini atakuwa anajua mchango wa Mzamiru Yassin katika nafasi ya kiungo kwenye klabu ya Simba. Tangu aliposajiliwa akitokea Mtibwa Sugar FC yapata miezi 16 iliyopita, Mzamiru amekuwa mtengenezaji wa nafasi nyingi za kufunga magoli kwa timu yake, wakati mwingine akiibuka katika nyakati zisizotarajiwa kwenye mchezo na kufunga magoli muhimu na ya kuvutia.
Licha ya kuhusika katika magoli yasiyopungua kumi msimu uliopita, kiungo huyo wa kati aliweza kufunga magoli nane katika ligi kuu-manne nyuma ya mfungaji bora wa klabu, Shiza Kichuya. Ni mzuiaji mzuri katikati ya uwanja na kitendo cha yeye kupita katika mikono ya walimu Hussein Mau, Allan Sigo wakati akiwa kinda kumefanya kumjenga kiupigaji pasi.
Ukifuatilia kwa umakini kuhusu wachezaji wengi waliotokea Moro Youth Soccer Academy utaona hata wale wa nafasi ya ulinzi kama Hassan Kessy, Salim Mbonde na wengine wanapenda kucheza mchezo wa kupiga sana pasi hasa zile za chini.
Mzamiru anacheza kama vile namba nane anavyotakiwa-kuunganisha timu kutokea nyuma hadi safu ya mashambulizi. “Unaona ile milingoti miwili ya goli?” ni swali ambalo nilipata kuulizwa yapata miaka 14 iliyopita na mwalimu Allan Sigo. Tulikuwa tumesimama wawili katikati ya uwanja huku mazoezi yakiendelea kama kawaida.
“Namba 8 mzuri ni yule anayecheza ndani ya milingoti minne ya magoli-goli A na goli B. Unapozuia hakikisha unafanya hivyo ukiwa ndani ya eneo lako, unaposhambulia hakikisha unacheza ndani ya eneo lako hii ni kwa sababu mpira unachezwa zaidi katikati ya uwanja na kitendo cha wewe kuwa nje ya eneo la kati kunatoa nafasi ya wazi kwa mpinzani wako kutawala mchezo akiwa huru,” maelezo haya niliyashika na nikayafanyia kazi.
Matokeo yake yalifaa kwangu hadi kwa timu kiujumla. Mzamiru anapita katika njia zile ambazo vijana wengi wa Morogoro waliopita katika mikono ya Moro Youth (Moro Kids ) walizofundishwa. Huyu ni namba 8 ambaye muda wote mchezoni hutumia kubaki eneo lake, anaposhambulia hutokea kati-fuatilia hata aina ya magoli yake anayobahatika kufunga. Hufunga kwa sababu huwa eneo sahihi muda wote, lakini anapaswa kujiongeza ili kuwa bora mara mbili ya alivyo sasa.
Kucheza kikubwa
Nilidhani uwezo wa Muzamiru ungekua zaidi msimu huu, lakini licha ya wengi kutoona ‘jicho langu la tatu’ linaona kuanza kushuka kwa uwezo wake. Hadi sasa hajafunga wakati ligi ikiwa raundi ya 11, hajatengeneza magoli ya kutosha japo hii si sababu za kushuka kwake bali uchezaji wake umekosa umakini.
Kwa mchezaji wa nafasi yake kupoteza pasi tatu kati ya tano anazopiga ni hatari na inahitaji uvumilivu mkubwa kwa kocha ili kuendelea kumpa nafasi mchezaji wa aina hiyo labda katika kikosi ambacho hakina ‘mbadala’ mwenye ubora. Katika michezo ya timu ya Taifa ya Tanzania Bara katika michuano ya Cecafa Challenge Cup 2017-Kenya, Mzamiru ni kati ya watu ambao wanapaswa kupewa lawama kwa kiwango cha chini kilichoonyeshwa na Kilimanjaro Stars.
Alikosa hamasa, alishindwa kupeleka mpira mbele, alipiga pasi nyingi zilizokuwa zikipotea ama kwenda kwa wachezaji wa timu pinzani. Licha ya kwamba amekuwa akitumia vizuri nguvu zake katika uporaji wa mpira na ukabaji, Muzamiru amekuwa akicheza ‘kitoto-toto’ mno wakati ni mchezaji ambaye makocha wake klabuni na katika timu za Taifa wanahitaji kujenga msingi wa kushambulia kwa timu zao kupitia yeye.
Anapaswa kubadili mtazamo wake kiuchezaji na kucheza kama mchezaji aliyepevuka na mwenye tamaa ya kupata matokeo bora kwa timu yake.

Kama atajipevusha kiuchezaji Mzamiru ni mchezaji ambaye amekamilika kama namba 8. Kwa sasa bado. Ningekuwa na CD ningemuonyesha vitu vya Shekhan Rashid ama Primus Kasonso ila inanibidi tu nimkumbushe kuwajibika zaidi na kujikuza kimpira. Anategemewa Simba na Stars.

No comments