Mgonjwa apasuliwa Ubongo kimakosa
Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta nchini Kenya ametumwa kwenye likizo ya lazima baada ya mgonjwa ambaye hakufaa kufanyiwa upasuaji wa ubongo kufanyiwa upasuaji huo katika hospitali hiyo.
Hatua ya kumpa likizo Lilly Koros kwenye likizo ya lazima imetangazwa na Waziri wa afya Sicily Kariuki ambaye amesema hatua hiyo inakusudiwa "kupisha uchunguzi".
Kisa hicho ambacho kimewashangaza wengi kilitokea katika hospitali hiyo wiki iliyopita na leo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa maafisa wa matibabu ambao walihusika kueleza ilikuwaje hadi kosa hilo likatokea.
Taarifa ya Bi Koros iliyotolewa Alhamisi ilisema maafisa wanne wa matibabu walikuwa wamesimamishwa kazi, akiwemo msimamisi wa sajili ya watu wanaofanyiwa upasuaji wa ubongo.
Wengine ni mwuguzi aliyekuwa akisimamia wadi, mwuguzi wa kuwapokea wagonjwa kwenye chumba cha kufanyiwa upasuaji na afisa wa kuwatia ganzi wagonjwa.
Bi Koros alisema kupitia taarifa kwamba kosa hilo lilitokea pale mkanganyiko ulipotokea kuhusu wagonjwa wawili waliokuwa hawajitambui.
Mmoja kati yao ndiye alihitaji upasuaji wa kichwa ili kuondoa damu iliyokuwa imeganda kwenye ubongo wake.
Huyo mwingine alikuwa amefurwa kwenye kichwa lakini alihitaji matibabu ambayo hayakushirikisha upasuaji.
Lakini asiyehitaji upasuaji ndiye aliyeishia kufanyiwa upasuaji. Madaktari waligundua kosa hilo saa chache baada yao kuanza upasuaji walipogundua kwamba hawakuweza kuiona damu iliyoganda kwenye ubongo wa mgonjwa waliokuwa wanamfanyia upasuaji.
Bi Koros ameomba radhi na kusema "tunafurahi kuwatangazia umma kwamba mgonjwa huyo sasa ametibiwa na anaenedelea vizuri kupata nafuu".
Wakenya walivyopokea habari hizo
No comments