Sweden, Kuwait zapendekeza azimio mgogoro wa Syria
Sweden na Kuwait zimependekeza kufanyike kura juu ya Azimio la Umoja wa Mataifa la usitishwaji wa mapigano wa siku 30 nchini Syria ili kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji pamoja na zoezi la kuwaondoa raia wagonjwa na waliojeruhiwa vibaya.
Azimio hilo lililopendekezwa linaelezea hasira juu ya viwango visivyokubalika vya vurugu na mashambulizi dhidi ya raia, hususan katika majimbo ya Idlib na eneo linalodhibitiwa na waasi la Ghouta Mashariki.
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema watu 346 wameuawa huko Ghouta tangu serikali ya Syria na washirika wake walivyoongeza mashambulizi makali Februari 4.
Urusi, ambayo ni mshirika muhimu kwa Syria imeitisha mkutano wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo Alhamis kuhusu Ghouta Mashariki. Ikiwa Urusi itatumia kura yake ya veto au kukwepa kupigia kura pendekezo hilo ni suala ambalo bado halijafahamika.
No comments