TUMBATU FM

Breaking News

Prisons na Stand United nazo zatinga Robo Fainali Azam Sports Federation Cup



TIMU za Tanzania Prisons na Stand United zimekamilisha idadi ya timu nane za kucheza hatua Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi kwenye mechi zao za leo.

Mapema mchana, Tanzania Prisons kutoka Mbeya ilipata ushindi wa 1-0, bao pekee la Ramadhani Ibata dhidi ya wenyeji, Kiluvya United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Na jioni, Stand United wakapata ushindi wa penalti 4-3 baada ya sare ya 0-0 na Dodoma FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Prisons na Stand United zinaungana na JKT Tanzania, Yanga SC, Mtibwa Sugar, Azam FC, Singida United na Njombe Mji FC zilizotangulia kufuzu Nane Bora ya ASFC.

Jana JKT Tanzania iliitoa Ndanda FC kwa kuichapa 2-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Yanga iliichapa Maji Maji 2-1 Uwanja wa Maji Maji mjini Songea jana na Mtibwa Sugar iliifunga 3-0 Buseresere FC Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.

Juzi Azam FC iliichapa KMC ya Kinondoni 3-1 Chamazi, Singida United iliilaza 2-0 Polisi Tanzania Uwanja wa Namfua, Singida juzi na Njombe Mji FC iliyowatoa Mbao FC Jumatano iliyopita kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1 Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.

Droo ya Robio Fainali inatarajiwa kupangwa wiki hii katika studio za Azam TV, Tabata mjini Dar es Salaam.

No comments