TUMBATU FM

Breaking News

Hizi ndio Hoja sita za Lissu kuhusu hukumu ya Sugu



Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu ameibua hoja sita kuhusu  hukumu ya mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu.

Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga Jana Februari 26, 2018 wamehukumiwa kifungo cha miezi mitano gerezani kwa kosa la kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Katika waraka wa Lissu ambaye pia ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) juu ya hukumu hiyo alioutoa Jana Februari 26, 2018 amesema, “waheshimiwa wangu salaam kutoka Ubelgiji. Nawapeni pole nyingi kwa yaliyomkuta Sugu na Masonga siku ya leo. Naomba kuzungumzia suala hili kwa kirefu kidogo.”

Katika hoja ya kwanza amesema, hukumu hiyo si  mwisho wa mjadala mahakamani na kwamba bado kuna fursa na haki ya rufaa Mahakama Kuu na ikibidi Mahakama ya Rufaa.

Pili, amesema hukumu hiyo haina maana Sugu atakaa gerezani muda wote, kwamba kuna haki ya dhamana (pending appeal) na kubainisha kuwa hivyo ndivyo walivyofanya kwa viongozi na wanachama wengi wa Chadema.

Katika hoja ya tatu, Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema amesema hukumu ya Sugu haina athari yoyote kwa mbunge huyo kuhusu kugombea tena ama kupoteza ubunge wake kwa sababu Katiba inaweka masharti ya kifungo cha miezi sita au zaidi na kwa makosa ya utovu wa uaminifu.“Uchochezi au kutoa lugha ya matusi sio makosa ya utovu wa uaminifu,” amesema.

“Nne, pamoja na kwamba sijaona nakala ya hukumu, adhabu ya kifungo bila faini kwa kosa la kwanza ni kinyume na ‘sentencing principles’. Hii ni mojawapo ya hoja zetu zilizoshinda katika kesi ya Peter Lijualikali (mbunge wa Chadema Kilombero) Mahakama Kuu mwaka jana,” amesema.

Tano, Lissu amesema hata kama Sugu atakaa gerezani muda wote huo (wa miezi mitano), hukumu za kesi za kisiasa kama hiyo hazijawahi kuwapunguzia heshima wapigania haki popote pale duniani.

“On the contrary (kinyume chake) kifungo cha aina hii ni beji ya heshima kwa kila mpigania haki na uhuru. Orodha ya mifano ni ndefu sana wapo akina  Nyerere (Julius-Rais wa Awamu ya Kwanza) japokuwa yeye alilipa faini, Kenyatta (Jomo-Rais wa zamani wa Kenya), Mandela (Nelson-Rais wa zamani wa Afrika Kusini), Mugabe (Robert-Rais mstaafu wa Zimbabwe), Fidel Castro (Rais wa zamani wa Cuba),” amesema.

Amesema alichokifanya hakimu leo katika kesi ya Sugu na Masunga ni kuwaongeza washtakiwa hao  kwenye orodha ya heshima hiyo.

Jambo la sita, Lissu amesema, “naunga mkono pendekezo la Zitto (Kabwe-Mbunge wa Kigoma Mjini)  kwamba wabunge wetu wote warekodi maneno aliyofungiwa nayo Sugu na kuyaweka mitandaoni ili watukamate na sisi pia, mpaka wakimbie wenyewe au watukamate na kutufunga wote.”

Amesema na sio wabunge tu, wahamasishe kila mwanachama na kila anayechukizwa na uonevu ayarudie maneno hayo ili nao wakamatwe na kufungwa.

No comments