Wanawake waliovalishana pete ya uchumba waachiwa kwa dhamana
Washtakiwa wanne katika shauri la kufanya vitendo vinavyoashiria
mapenzi ya jinsia moja na makosa la kimtandao wameachiwa kwa dhamana baada ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza kutupilia mbali hoja za kuzuia dhamana zao
zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi,
Wilbert Chuma leo Desemba 15, baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wa
utetezi, Mashaka Tuguta, Ogastini Kulwa na Jebra Kambole kuwa hoja
zilizowasilishwa na upande wa mashtaka ni dhaifu mbele ya macho ya sheria.
Washtakiwa katika shauri hilo namba 548/2017 ni Milembe Suleiman
na Janeth Shonza wanaodaiwa kuvishana pete ya uchumba licha ya wote kuwa
wanawake.
Wengine ni Aneth Mkuki anadaiwa kufanikisha sherehe wawili hao
kuvishana pete na Richard Fabian anayeshtakiwa kwa kosa la mtandao kwa
kusambaza video za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii.
Katika uamuzi wake, Hakimu Chuma amesema Mahakama haiwezi
kufanyia kazi maelezo na vitu vya mashaka na uvumi kuwa washtakiwa wanaweza
kudhuriwa na jamii iliyochukizwa na kitendo wanachoshtakiwa nacho.
“Ni uamuzi wa Mahakama kuwa dhamana ni haki ya washtakiwa na
upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha hoja za msingi kwa nini wanyimwe
dhamana zaidi ya kutoa hoja za hisia kuwa wakiachiwa watadhuriwa na jamii bila
kueleza watadhurikaje na nani haswa atawadhuru,” amesema Hakimu Chuma katika
uamuzi wake
Washtakiwa wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya
kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho na barua ya utambulisho
kutoka mamlaka inayotambulika kisheria pamoja na kusaini hati ya dhamana ya Sh6
milioni. Shauri limeahirishwa hadi Januari 8, mwakani.
Chanzo: MWANANCHI
No comments