JELA MIAKA 20 KWA KUKAMATWA NA NYAMA YA KIBOKO
Mahakama ya wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi imemhukumu Omary Maganga (45) mkazi wa kijiji cha Itenka Rarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda kutumikia jela kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukamatwa na nyama ya Kiboko kilo 118.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali Fraviani Shio.
Awali katika kesi hiyo mwendesha mashtaka mwanasheria wa serikali Fraviani Shio alidai Mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Omary Maganga alitenda kosa hilo Oktoba 10 mwaka 2016 majira ya saa kumi jioni.
Alidai kuwa siku hiyo ya tukio mshitakiwa alikamatwa akiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi huku akiwa na nyama ya kiboko yenye uzito wa kilo 118 yenye thamani ya Tshs 3,274,500.
Mwanasheria huyo wa Serikali aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa huyo alikamatwa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi baada ya kuwa wamepata taarifa kutoka kwa raia wema za kuwa mshitakiwa amekuwa akifanya ujangili kwenye hifadhi ya Taifa na ndipo walipoanza msako na kufanikiwa kumkamata siku hiyo akiwa ndani ya Hifadhi ya Katavi huku akiwa na nyama hiyo ya Kiboko.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Chiganga alisema kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo na upande wa mashitaka ambao ulikuwa na mashahidi watano na na mshitakiwa hakuwa na shahidi yoyote alisema Mahakama pasipo mashaka yoyote imemwona mshitakiwa akiwa amepatikana na hatia ya kifungo cha sheria Namba 86 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha sheria ya wanyama pori Namba 5 ya mwaka 2009.
Hivyo kabla ya kusoma hukumu alitowa nafasi kwa mshitakiwa ya kuweza kujitetea na kama anayo sababu yoyote ya msingi ya kuweza kuishawishi mahakama iweze kumpunguzia adhabu.
Mshitakiwa Maganga katika utetezi wake aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kwa kile aichodai hilo lilikuwa ni kosa lake la kwanza katika maisha yake na pia anayo familia ambayo inamtegemea ya mke na watoto pamoja na wazazi wake .
Utetezi huo ulipingwa vikali na mwanasheria wa Serikali Fraviani ambae aliiomba Mahakama itowe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kuhujumu uchumi wa nchi.
Hakimu Chiganga Ntengwa baada ya kuzisikiliza mbili aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa Omary Maganga kutokana na makosa yaliomtia hatiani Mahakama imemuhukumu kutumikia jela kifungo cha miaka 20 kuanzia jana na kama haja ridhika na adhabu hiyo inayonafasi ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya juu zaidi .
No comments