Jamii nchini imeshauriwa kujitokeza kupima afya zao ili kufahamu kama kuna viashiria vya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ili kupatiwa tiba mapema.
Ushauri huo umetolewa na Meneja wa Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (NCD) Dkt Omar Muhamed Suleiman wakati walipokuwa wakiendesha zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi katika Kitengo cha maradhi hayo Hospitali ya Mnazimmoja.
Amesema kuwa ugonjwa huo ni tishio kubwa duniani kote kutokana ripoti yaShirika la Afya Ulimwenguni (WHO) inakadiria kuwa zaidi ya wanawake 275,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo ambapo idadi kubwa ya watu hao ni kutoka nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Aidha amefahamisha kuwa iwapo saratani hiyo itagundulika katika hatua za awali ni rahisi kutibika na kupona kabisa hivyo Wizara imeamua kuanzisha uchunguzi huo hatua kwa hatua ili wananchi kuweza kujigundua nmapema na kupatiwa matibabu.
Nao wananchi waliyofanyiwa uchunguzi huo wameiomba Serikali kuendelea kushirikiana na wafadhili mbalimbali katika sekta ya afya ili kuwapatia tiba kwani kufanya hivyo kunawapunguzia gharama za matibu.
Wamefahamisha kuwa hapo nuyma walikuwa wakipata shida kutokana na matibabu ya ugonjwa huo kuwa hayapatikani Zanzibar lakini kwa sasa wamekua wakipatiwa tiba hizo mara kwa mara jambo ambalo limewaondoshea usumbufu waliokuwa wakiupata hapo kabla.
Aidha wamewashauri akina mama wenzao na wanawake kujitokeza kwa wingi kwenda kuangalia afya zao kwa kufanya uchunguzi wa maradhi mbalimbali kwani uchunguzi na matibabu hayo ni bure.
Uchunguzi wa maradhi hayo umeandaliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya wakishirikiana na Hospitali ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China .
No comments