Watanzania wameaswa kujitokeza  kushiriki katika Sensa  ya Watu na Makazi  Mwaka 2022 na Sensa ya Majaribio inayotarajiwa kufanyika Agosti  2021 ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa takwimu  za sasa ambazo ni halisi na zinazoakisi mahitaji ya jamii kwa sasa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya  Walemavu  Mhe. Ummy  Nderiananga kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu   Nchemba. wakati akifungua kikao kazi cha  Wadau kutoa maoni kwenye dodoso la Sensa   ya mwaka 2022

Amesema kuwa Serikali imejipanga na inaomba wadau wote kuunga mkono utekelezaji wa mipango yote iliyopangwa katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi wake.

Aidha, Mhe Nderiananga  amewataka washiriki wa kikao kazi hicho cha kutoa maoni kushiriki kikamilifu na kujiepusha  kuingiza siasa katika kutoa maoni yao ili kufanikisha dhamira  na matakwa ya kisheria yakuwashirikisha wadau katika mchakato wa kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha dodoso litakalotumika katika Sensa mwaka 2022.

Katika kikao hicho Mhe. Nderiananga amewahimiza  watanzania kutoa ushirikiano katika mchakato mzima wa Sensa kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan Wakati akifungua mkutano wa Jumuiya ya Kikristu mjini Morogoro hivi karibuni.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango  Dkt.  Khatib   Kazungu amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Sensa ya Watu na Makazi inafanyika  kama ilivyopangwa na kutoa wito kwa wadau wa ndani na  nje ya nchi kushirikiana na Serikali kufanikisha Sensa hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NBS Dkt. Amina Msengwa amesema kuwa wamepokea maelekezo  yote yaliyotolewa na mgeni rasmi na watayafanyia kazi kwa kuzingatia umuhimu  wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Aliongeza kuwa Bodi ya NBS na Menejimenti iko imara katika kuhakikisha kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inafanyika kwa ufanisi na inafanikiwa kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) Dkt. Victor Bakengesa   amesema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Awali akieleza umuhimu wa kikao cha wadau kutoa maoni kuhusu dodoso la Sensa ya mwaka 2022, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa maoni yanayokusanywa yatasaidia kuleta tija katika kufanikisha Sensa hiyo.

Aliongeza kuwa mkutano huo wa wadau ni wakwanza na utafuatiwa na mikutano mingine kama hiyo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya sheria  ya Takwimu Sura 351.

Sensa ya Watu na Makazi inatarajiwa kufanyika mwaka 2022 kote nchini na itatatunguliwa na Sensa ya majaribio mwezi Agosti 2021.