TUMBATU FM

Breaking News

mamlaka ya DPP kuzuia dhamana Mahakama yatoa uamuzi mwingine



Mahakama ya Rufaa imesema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anapowasilisha hati kuzuia dhamana kwa washtakiwa kwa kukidhi matakwa ya kisheria mahakama inakuwa imefungwa mikono.

Uamuzi huo umetolewa siku chache baada ya Mahakama hiyo Februari 2 kutoa hukumu iliyomwondolea DPP mamlaka ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa bila hata kulazimika kutoa sababu, baada ya kubatilisha kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, kinachompa mamlaka hayo.

Katika hukumu ya Februari 23 kuhusu rufaa iliyokatwa na aliyekuwa mwanasheria wa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco), Emmanuel Massawe, Mahakama imesema DPP anapowasilisha hati ya zuio la dhamana dhidi ya mshtakiwa, hata mahakama inakuwa imefungwa mikono isipokuwa tu, kama itathibitika kuwa DPP alichukua uamuzi huo kwa nia mbaya. Massawe alikata rufaa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na Jaji Isaya Arufani Aprili 12, 2016.

Katika maombi hayo namba 51 ya mwaka 2016, Massawe na wenzake waliomba dhamana licha ya DPP kuizuia chini ya kifungu cha 36 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Mahakama Kuu ilikataa kutoa dhamana ikieleza DPP anapowasilisha hati kuzuia dhamana chini ya kifungu cha 36 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, mahakama inakuwa haina mamlaka ya kuitoa.

Massawe, kupitia jopo la mawakili Dk Rugemeleza Nshalla, Fulgence Massawe na Jeremiah Mtobesya, alikata rufaa Mahakama ya Rufaa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu wakitumia hukumu ya mahakama hiyo iliyobatilisha kifungu cha 148 (4) cha CPA.

Kifungu hicho kinampa DPP mamlaka ya kuizuia Mahakama au ofisa wa Polisi kutoa dhamana kwa mshtakiwa au mtuhumiwa baada ya kuwasilisha hati ya maandishi, kwa maelezo kuwa usalama au masilahi ya Jamhuri yataathirika.

Awali, Mahakama ya Rufaa katika hukumu ya Februari 2 ya rufaa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya mwanaharakati wa haki za binadamu, Mtobesya alisema kifungu hicho ni kinyume cha Katiba na ni batili.

Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watano wa Mahakama ya Rufaa waliokubaliana na ya awali iliyotolewa na Mahakama Kuu. Majaji waliosikiliza na kutoa hukumu ya rufaa hiyo ni Bernard Luanda (kiongozi wa jopo), Kipenka Mussa, Bethuel Mmila, Stellah Mugasha na Jacob Mwambegele.

Mahakama katika rufaa ya Massawe imeitupilia mbali ikikubaliana na hoja za Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuwanyima dhamana washtakiwa.

Hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Richard Mziray kwa niaba ya jopo la majaji watatu walioisikiliza wakiongozwa na Mbarouk Mbarouk na Rehema Mkuye ilisomwa Ijumaa iliyopita na naibu msajili wa Mahakama ya Rufaa, Amir Msumi.

Katika hukumu hiyo ambayo Mwananchi imeiona nakala yake, majaji hao wanasema ingawa mawakili katika hoja zao walijaribu kuishawishi Mahakama itoe uamuzi kwa kufuata kesi ya Mtobesya, haiwezi kutumika kwenye rufaa hiyo kwa kuwa ni mashauri mawili tofauti.

Majaji hao wamesema rufaa ya Mtobesya ilikuwa ya Kikatiba ikihoji uhalali wa kifungu kinachompa mamlaka DPP kuzuia dhamana, wakati katika rufaa ya Massawe anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu kumnyima dhamana.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Mahakama imesema ilibaini kuwa hoja ya msingi iliyotawala mjadala wa hoja za mawakili ni iwapo hati ya DPP aliyoiwasilisha mahakamani chini ya kifungu cha 36 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kuzuia dhamana kwa maelezo kuwa itaathiri masilahi ya Jamhuri inatosha kuwanyima dhamana.

Majaji katika hukumu hiyo wanasema Mahakama inakubaliana na wakili wa Serikali, Kweka kuwa DPP anapowasilisha hati ya zuio la dhamana dhidi ya mshtakiwa, hata Mahakama inakuwa imefungwa mikono isipokuwa tu kama itathibitika kuwa alichukua uamuzi huo kwa nia mbaya.

Wamesema Mahakama ilishaweka masharti matatu ya msingi ya hati ya DPP ya zuio la dhamana chini ya kifungu cha 36 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, katika kesi ya DPP dhidi ya Nuru Dirie na mwenzake, katika taarifa za sheria za mwaka 2002 (TLR).

Masharti hayo yanatajwa kuwa ni; DPP lazima awasilishe hati ya maandishi; ieleze sababu kuwa usalama na masilahi ya umma yataathirika kwa kutoa dhamana kwa washtakiwa; na hati hiyo ni lazima ihusiane na kesi ya jinai ama inayosubiri kusikilizwa au inayosubiri rufaa.

Hukumu hiyo inaeleza masharti hayo yalithibitishwa na Mahakama katika kesi ya rufaa ya DPP dhidi ya Li Ling Ling ya 2015 .

Majaji hao wamesema hati ya DPP inaweza tu kuwa batili inapothibitika kwamba alifanya hivyo kwa nia mbaya au matumizi mabaya ya utaratibu wa kimahakama, jambo ambalo halikuwa hoja katika rufaa hiyo.

No comments