Chirwa awafungukia Mashabiki
STRAIKA mahiri wa kupachika mabao wa Yanga, Mzambia, Obrey Chirwa amewahoji mashabiki wa soka waliokuwa wakimuambia aachane na Yanga ili aende Simba kwa kuwaambia: “Niende Simba kufanya nini?”
Ishu hii imekuja baada ya taarifa kuwepo zikimhusisha straika huyo na mipango ya kujiunga na Simba baada ya madai kuwa amekuwa akiidai Yanga fedha za usajili na mshahara.
Chirwa ambaye ni majeruhi kwa sasa, alikuwa akiulizwa maswali kadhaa na mashabiki wake live kupitia Mtandao wa Kijamii wa Instagram.
Straika huyo mwenye mabao 11, hajaungana na kikosi cha Yanga ambacho jana Jumapili kilicheza na Majimaji katika mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 16 bora kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
“Mnaniuliza niende Simba! Simba niende kule kufanya nini au kuna nini? Mniache na Yanga yetu, tutaendelea kupambana mpaka mwisho tu,” alisema Chirwa na kuwataka mashabiki waachane na maswali ya hivyo.
Hata hivyo, Chirwa aliulizwa maswali kadhaa huku mengine akionekana kuwapotezea mashabiki wake, hasa lile la kwa nini amekuwa akikosa penalti mara kwa mara huku wengine wakimshauri aachane na Yanga kwa kuwa hawana fedha ya kumlipa lakini hakuweza kujibu maswali hayo.
No comments